Halmashauri ya kitaifa ya kukabiliana na mihadarati na utumizi mbaya wa pombe (NACADA), imetoa wito kwa viongozi wa kidini, kupiga vita matumizi ya mihadarati katika mahubiri yao, ili kuokoa kizazi kijacho.
Mshirikishi wa halmashauri hiyo katika kaunti za Siaya na Busia Ken Marau, alisisitiza kuwa jukumu kuu la taasisi za kidini ni kutoa mwongozo wa kimaadili na kushughulikia janga la utumizi wa mihadarati.
Akizungumza mjini Siaya baada ya warsha ya siku moja uliowaleta pamoja viongozi wa kidni katika eneo hilo, Marau aliwahimiza viongozi hao kuimarisha juhudi za kukabiliana na utumizi wa dawa za kulevya.
“Wakati umewadia kwa viongozi wa kidini kutoa mwongozo wa kimaadili kwa jamii,” alisema Marua huku akidokeza kuwa NACADA itaendelea kushirikiana na washirika wengine kutokomeza jinamizi la utumizi wa mihadarati hapa nchini.
Wakati huo huo mshirikishi huyo wa NACADA, alitoa wito kwa washirika kutoa habari mwafaka kwa asasi husika ili kusaidia kukabiliana na uovu huo.