Viongozi wa Azimio kukutana kupanga mikakati ya maandamano

Marion Bosire
1 Min Read

Kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement Kalonzo Musyoka, amesema kwamba viongozi wakuu wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya watafanya kikao leo Jumatatu kupanga mikakati ya maandamano ya Jumatano.

Akizungumza katika kanisa la Missioners of Hope Christ Ministries, huko Utawala, eneo bunge la Embakasi Mashariki, Kalonzo alisema baada ya mkutano wao, viongozi hao wa Azimio watawapatia wafuasi wao mwelekeo.

Kalonzo pia alishtumu serikali ya Kenya Kwanza akisema haijali vilio vya wakenya kuhusu kiwango cha juu cha ushuru na gharama ya maisha inayozidi kupanda.

Kulingana naye, serikali imeonyesha kiburi kwa jinsi inachukulia wakenya kila wanapojaribu kuzungumzia matatizo yao.

Alishtumu baadhi ya viongozi serikalini waliodai kwamba Kenya ni kampuni na ina wenye hisa na kuongeza kwamba wakati umewadia wa kila mkenya kupatiwa hisa zake.

Kalonzo alishukuru maafisa wa polisi katika kaunti ya Machakos ambao anasema walionyesha uvumilivu na kukubalia maandamano na mikutano ya amani wakati wa maadhimisho ya siku ya Saba Saba.

Alionyesha kutoridhika na yaliyojiri bungeni wakati wa kupitishwa kwa mswada wa fedha wa mwaka huu ambapo mbinu mbali mbali zilitumika kushinikiza wabunge kuupitisha.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *