Viongozi serikalini na Wakenya mbioni kupanda miti

Martin Mwanje
1 Min Read

Viongozi mbalimbali serikalini leo Jumatatu walidamka wakiwa katika ari ya kushiriki zoezi la kitaifa la upanzi wa miti. 

Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei aliongoza zoezi la upanzi wa miti katika kaunti ya Nairobi.

“Yeyote anayepanda miti, anapanda matumaini. Kufuatia azima ya serikali ya kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032, leo asubuhi, niliongoza zoezi la upanzi wa miti katika kaunti ya Nairobi, nikianza na Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Kasarani,” alisema Koskei punde baada ya kuongoza zoezi hilo.

Huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya, KCGS yenye makazi yake katika kaunti ya Turkana ilianza zoezi la upanzi wa miti katika eneo la Lowarengak.

“Kilele cha zoezi hilo kitakuwa katika eneo la Mikindani Tudor Creek, ambako miti 100,000 itapandwa,” ilisema KCGS.

Kwenye vilima vya Ngong, wawakilishi wa shirika la utangazaji nchini, KBC walikuwa mbioni kupanda miti kupiga jeki juhudi za serikali za kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

Serikali imetangaza leo Jumatatu kuwa sikukuu ya upanzi wa miti kote nchini huku miti milioni 500 ikilengwa kupandwa siku hiyo.

Rais William Ruto atazindua zoezi la kitaifa la upanzi wa miti katika eneo la Makindu, kaunti ya Makueni.

 

Share This Article