Viongozi mbalimbali wamezidi kummiminia sifa Naibu Rais mteule Prof. Kithure Kindiki.
Kuteuliwa kwa Prof. Kindiki kwenye wadhifa huo kumetangazwa leo Ijumaa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula.
Hii ni baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Rais William Ruto ikibainisha kuwa amemteua Prof. Kindiki kwenye wadhifa huo ulioachwa wazi na mtangulizi wake Rigathi Gachagua.
“Pongezi Ndugu yangu Prof. Kithure Kindiki kufuatia uteuzi wako kama Naibu Rais. Hudumu kwa uadilifu, kujitolea na kwa bidii ya mchwa kuliunganisha taifa chini ya bendera moja na kulisongesha mbele taifa,” alisema Kimani Ichung’wah, kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa kupitia mtandao wa X.
“Fanya kazi bila kuchoka, kwa kujitolea na dhamira, ukilenga kuhakikisha maendeleo, umoja na ustawi wa watu wote.”
Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru pia amemlimbikizia sifa Prof. Kindiki kufuatia uteuzi wake.
“Ndugu yangu Prof. Kithure Kindiki, pongezi zangu za dhati. Kwako, historia imekutwika heshima na wajibu wanaopata watu wachache tu,” alisema Waiguru katika taarifa.
“Mwenyezi Mungu akuongoze pamoja na Rais William Ruto kuiongoza nchi hii tukufu kufikia upeo wake wa maendeleo.”
Uteuzi wa Prof. Kindiki kuwa Naibu Rais unafuatia hatua ya jana Alhamisi usiku ya Bunge la Seneti kumtimua Rigathi Gachagua kwenye wadhifa huo.
Hii ni baada ya Maseneta kupitisha mashtaka 5 kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi ya Gachagua katika hoja maalum iliyopitishwa na Bunge la Taifa hapo awali.
Hoja hiyo iliyopitishwa na wabunge 281 iliwasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Bunge la Taifa sasa linatarajiwa kumpigia msasa Prof. Kindiki na ikiwa bunge litaridhia uteuzi wake, basi atateuliwa rasmi na Rais kuhudumu kwenye wadhifa huo.