Kiungo mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Vinícius Paixao de Oliveira Júnior, anapigiwa upato kutawazwa mshindi wa tuzo ya mwanandinga bora wa soka mwaka huu, maarufu kama Ballon d’Or kwa wanaume.
Makala ya mwaka huu ya tuzo hiyo yataandaliwa jijini Paris, Ufaransa, Jumatatu usiku.
Vinícius aliye na umri wa miaka 24 alikuwa na msimu wa kufana mwaka jana, akiisaidia Madrid kutwaa ubingwa wa Ulaya na pia ligi kuu Uhispania maarufu kama La Liga.
Tuzo ya mwaka huu kwa wanaume kwa mara ya kwanza haina Lionel Messi wala Cristiano Ronaldo ambao wametawala tuzo zilizopita 10.
Wengine walio kwenye orodha hiyo ni chipukizi wa Barcelona Lamine Yamal wa Uhispania, Jude Bellingham wa Uingereza na Real Madrid, Hakan Çalhanoğlu wa Uturuki na Inter Milan, Dani Carvajal wa Uhispania na Real Madrid, Rúben Dias wa Ureno na Manchester City na Artem Dovbyk wa Ukraine.
Wawaniaji wengine ni Phil Foden wa Manchester City,Alejandro Grimaldo wa Bayer Leverkusen,Erling Haaland wa Manchester City,Mats Hummels wa Borussia Dortmund,Harry Kane wa Bayern Munich,Toni Kroos wa Real Madrid,Ademola Lookman wa Atalanta,Emiliano Martínez kutoka Aston Villa,Lautaro Martínez wa Inter Milan,Kylian Mbappé aliyekuwa wa Paris Saint-Germain,Martin Ødegaard wa Arsenal,Dani Olmo wa Barcelona,Cole Palmer wa Chelsea,Declan Rice wa Arsenal,Rodri wa Manchester City,Antonio Rüdiger wa Real Madrid,Bukayo Saka na William Saliba wote kutoka Arsenal.
Orodha hiyo pia inawajumuisha Federico Valverde wa Real Madrid, Vitinha wa Paris Saint-Germain, Nico Williams kutoka Athletic Club, Florian Wirtz wa Bayer Leverkusen, na Granit Xhaka wa Bayer Leverkusen.
Messi na Aitana Bonmati wa Uhispania walitawazwa washindi wa tuzo hiyo kwa wanaume na wanawake mwaka jana mtawalia.