Malumbano yaliyoshuhudiwa katika bunge la kaunti ya Machakos siku ya Jumanne, yamesababisha vikao vya bunge hilo kuahirishwa kwa muda usiojulikana.
Ghasia hizo zilizuka kati ya upande wa waliowengi na upande wa waliowachache katika juhudi za kumtimua spika wa bunge hilo Anne Kiusya.
Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Machakos, waliitwa kutuliza mgogoro kati ya upande wa wengi ulioogozwa na mwakilishi wadi ya Machakos ya kati Nicholas Nzioka, na upande wa waliowachache ulioongozwa na mwakilishi wodi ya Mua, Francis Ngunga.
Kizaazaa hicho kilizuka asubuhi wakati kamati ya shughuli za bunge ikiongozwa na spika Kiusya ilipokutana kupanga ratiba ya bunge.
Inadaiwa kuwa wabunge wanaompinga Kiusya, walivuruga kikao hicho wakilenga kuwasilisha hoja ya kumtimua.
Hata hivyo, kundi lingine la wawakilishi wadi, lililopinga kutimuliwa kwa spika huyo, liliwashambulia wenzao kutoka upande wa wengi na kusababisha ghasia zilizosababisha kujeruhiwa kwa wawakilishi wadi watatu.
Juma lililopita, Mahakama Kuu ya Machakos ilitoa agizo la kusimamisha mjadala wa kumuondoa mamlakani Spika wa bunge hilo, hadi Aprili 30, wakati ambapo swala hilo litasikizwa mahakamani.