Waziri wa leba na ulinzi wa jamii Dkt. Alfred Mutua,ametoa wito kwa vijana ambao hawana ajira, kutafuta ajira katika nchi za kigeni ili kuboresha maiasha yao.
Waziri huyo alidokeza kuwa kuna fursa nyingi za ajira katika mataifa ya kigeni, akiwamihiza vijana hao kuchukua fursa hiyo kwa lengo la kukabiliana na zimwi la umaskini hapa nchini.
Dkt. Mutua aliyasema hayo katika chuo cha kiufundi cha Wote (TTI),wakati wa zoezi la kuwasajili vijana wasio na ajira katika kaunti ya Makueni.
Waziri huyo aliwahimiza vijana ambao wametuma maombi ya kazi, kuhakikisha wanapata pasipoti, akisema serikali itaharakisha mchakato wa utoaji hati hiyo kuwawezesha kusafiri ng’ambo kwa ajira.
“Kuna fursa za kazi Ujerumani,Qatar na Poland. Hakuna haja ya kuwa na vijana ambao hawana ajira, wakati ambapo kuna nafasi za ajira ng’ambo,” alisema Dkt. Mutua.
“Ikiwa huna paspoti, serikali itahakikisha unapata hati hiyo katika muda wa siku mbili,” alidokeza waziri huyo.
Vijana waliochukuliwa waliishukuru serikali kwa fursa hiyo itakayowatoa katika lindi la umaskini.
Waziri huyo alikua ameandamana na kamishna wa kaunti ya Makueni Duncan Darusi, miongoni mwa maafisa wengine wakuu wa serikali.