Vijana ambao wametimiza umri wa miaka 18, na ambao hawana vitambulisho vya kitaifa wamehimizwa kutumia fursa ya kuondolewa kwa ada ya vitambulisho kujisajili ili kuvipokea.
Katibu wa usalama wa ndani Raymond Omollo anasema serikali iliondoa ada ambayo awali ilikuwa ya lazima ya shilingi 300, ili kuwezesha kila mkenya apate kitambulisho bila mzigo wowote wa kifedha.
Omollo ambaye alikuwa akizungumza huko Kuria Magharibi, kaunti ya Migori jana, alisema kwamba vituo vya Huduma kote nchini vinatoa vitambulisho vya kitaifa.
Kuhusu usajili unaoendelea wa wakenya katika mpango wa afya wa Taifa care chini ya mamlaka ya afya ya jamii SHA, Omollo alisisitiza umuhimu wa kujisajili akisema serikali itatumia deta hiyo kupanga masuala ya matibabu yao.
Alihimiza wale ambao bado hawajajisajili na wana uwezo kifedha wafanye hivyo na wahakikishe wanatoa michango yao ya kila mwezi bila kuchelewa.
Katibu Omollo vile vile alizungumzia kujitolea kwa serikali kuhakikisha amani inadumu katika mpaka wa pamoja wa kaunti za Migori, Kisii na Narok ambapo vurugu hushuhudiwa kila mara na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.
Alisema serikali kwa sasa inaendeleza mazungumzo na viongozi wa kaunti hizo tatu katika juhudi za kuafikia suluhu ya kudumu, huku usalama ukiimarishwa huko kuhakikisha hakuna maafa zaidi.