Vijana 1,500 huenda watanufaika pakubwa katika eneo maalum la kiuchumi la Naivasha, huku serikali ikilenga kubuni nafasi za ajira katika kiwanda cha utengenezaji wa magari yanayotumia nguvu za umeme.
Katibu katika wizara ya biashara na viwanda Abubakar Hassan Abubakar, alisema kiwanda cha kutengeneza magari cha Tad Motors, kitaanza shughuli zake katika eneo maalum la kiuchumi la Naivasha katika muda wa miezi sita ijayo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kampuni hiyo, katibu huyo, alisema serikali itatumia maeneo maalum ya kiuchumi nchini kuzindua nafasi za kazi kwa mamia ya vijana nchini.
“Uwekezaji huu utabuni nafasi 100 za ajira wakati wa ujenzi wa kiwanda hiki, na nafasi 1,500 wakati kitakapoanza shughuli zake katika muda wa miezi sita ijayo,” alisema Abubakar.
Kampuni hiyo ya Tad Motors, imewekeza dola milioni tatu kwenye eneo hilo la kiuchumi, kujenga kiwanda cha magari hayo yanayotumia nguvu za umeme, yatakayouzwa humu nchini na katika soko la kimataifa.