Vijana 15 walifikishwa katika mahakama ya Eldoret siku ya Jumatatu kujibu mashtaka ya uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024 juma lililopita.
Wakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Dennis Mikoyan, afisa wa uchunguzi Ekiru Kirimoni aliambia mahakama kuwa vijana hao wanachunguzwa kwa mashtaka kadhaa ikiwa ni pamoja na kuiba, kumiliki bidhaa zinazoshukiwa kuwa za wizi na uharibifu wa mali.
Polisi waliomba siku 21 ili kukamilisha uchunguzi huku vijana hao wakizuiliwa kwenye rumande.
Vijana walioshtakiwa walitambuliwa kuwa Vincent Ragila, Sheila Rotich, Ferdinand Lubisa, Annex Bahati, Eric Mulamba, Brian Kimeli na Martin Kabugi.
Wengine ni Alfred Oloo, Daniel Shananji, Stephen Omonji, Joshua Majimbo, Amos Kiprotich, Moses Simawatwa, Brian Rotich na Amon Lenny.
Wakili George Sunkule ambaye ni miongoni mwa wanaowakilisha vijana hao alikataa ombi la polisi la kuwazuilia, akisema kuwa tayari walikuwa wamezuiliwa kinyume cha sheria kwa zaidi ya saa 24 zinazohitajika kwa mujibu wa sheria bila kufunguliwa mashtaka.
Hakimu Mikoyan aliamuru vijana hao wazuiliwe katika korokoro ya Eldoret hadi Alhamisi atakapotoa uamuzi kuhusu ombi la polisi.
Wakati wa maandamano hayo, kilabu cha Timba Xo kinachomilikiwa na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi kiliharibiwa kwa kupigwa mawe na bidhaa kuporwa.
Zaidi ya maafisa Kumi walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo, huku magari kadhaa yakiharibiwa miongoni mwa mali nyingine.