Idadi ya vifo vilivyotokana na maporomoko ya ardhi katika jaa la taka jijini Kampala nchini Uganda vimeongezeka hadi 21 kulingana na maafisa wa polisi.
Waokoaji wanaendelea kupekua vifusi kutafuta manusura wa mkasa huo ambao Meya wa jiji la Kampala Erias Lukwago alisema ulitarajiwa.
Mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha jijini Kampala ilisababisha kuporomoka kwa vilima vya takataka ambavyo viliangukia nyumba zilizo karibu na kuzika watu waliokuwa wamelala Ijumaa usiku.
Katika taarifa, Rais Yoweri Museveni alisema ameelekeza waziri mkuu kuratibu kuondolewa kwa watu wanaoishi karibu na jaa hilo la taka.
Serikali ya nchi hiyo pia imeanzisha uchunguzi kuhusu mkasa huo na kilichousababisha na maafisa watakaobainika kuzembea kazini na watachukuliwa hatua kali.
Watu wapatao 14 wameokolewa kutoka eneo hilo kulingana na msemaji wa polisi nchini Uganda Patrick Onyango. Onyango alisema pia kwamba idadi isiyojulikana ya watu huenda bado wamekwama chini ya vifusi.
Jaa hilo la Kiteezi la ukubwa wa ekari 36 ndilo la pekee linalotumiwa na wakazi wote wa Kampala wapatao milioni nne na Meya Lukwago alisema maafisa wamekuwa wakitafuta eneo jingine la kutupa taka kwa muda sasa.