Vifaa vya mawasiliano “pagers” vimelipuka nchini Lebanon jana Jumatano kwa siku ya pili mtawalia.
Wizara ya Afya nchini humo imetangaza kuwa watu 14 wameuawa kutokana na milipuko hiyo huku watu zaidi ya 450 wakijeruhiwa.
Juzi Jumanne, watu 12 walifariki na zaidi ya 2,700 kujeruhiwa baada ya vifaa hivyo kulipuka nchini humo.
Kundi la Kiislamu la dhehebu la Shia lenye makao yake nchini Lebanon, Hezbollah limeinyoshea Israel kidole cha lawama kufuatia mashambulizi hayo na kuapa kutekeleza shambulizi la kulipiza kisasi.
Serikali ya Israel bado haijatoa tamko rasmi kuhusu mashambulizi hayo wakati uvumi ukirindima kuwa huenda yakaongeza mivutano Mashariki ya Kati.