Mkosoaji wa mitandaoni wa watu maarufu nchini Nigeria Vincent Martins Otse ambaye wengi wanamfahamu kama VeryDarkMan au VDM, amemkosoa mwanamuziki Burna Boy kutokana na alichokifanya jukwaani.
Mshindi huyo wa tuzo ya Grammy alikuwa jukwaani katika tamasha la “The Greater Lagos” la kukaribisha mwaka mpya ambapo aliamua kuondoka jukwaani baada ya shabiki kumkimbilia.
VDM alichapisha video nyingine inayoonyesha jinsi Burna Boy alimshughulikia shabiki mzungu awali akiwa ughaibuni akilinganisha na alivyomfanya shabiki wa nyumbani.
Burna anaonekana akimsalimia shabiki huyo mzungu, akampiga pambaja, akamuuliza jina lake kisha akaambia umati umshangilie kabla ya jamaa huyo kuondoka jukwaani.
Mkosoaji huyo anahisi Burna Boy alichukua hatua ambayo haikustahili lakini pia anamlaumu shabiki aliyeruka na kuingia jukwaani kwani chochote kingeweza kutokea.
“Alichokifanya Burna Boy ni makosa asilimia 1000 lakini hebu tujiulize maswali kadhaa. Huyo jamaa likuwa anafanya nini jukwaani? Hasa katika eneo kama Lagos? Ni kamera ngapi za ulinzi ziko Lagos?” alisema VDM kwenye video aliyochapisha.
Kwa jumla, VDM anahisi kwamba Burna Boy anadharau watu wa Nigeria akisema angemkwepa tu shabiki huyo na aendelee kutumbuiza badala ya kukatiza tumbuizo ghafla.
Burna Boy alikuwa amejieleza kupitia Instagram akisema aliondoka jukwaani kwa sababu kila mmoja anafahamu sheria zake kwamba hapendi kuingiliwa anapokuwa akitumbuiza.
Alisema pia kwamba ana tatizo la hisia pale anaposhtuliwa ndiposa hangeweza kuendelea kuimba.