Matumizi ya jumla ya data nchini Kenya yaliongezeka kwa asilimia 20.4 katika kipindi cha miezi mitatu hadi mwezi Machi mwaka huu.
Mamlaka ya Mawasiliano nchini, CA imehusisha hatua hiyo na kuongezeka kwa matumizi ya intaneti miongooni mwa watumiaji.
Hii inakuja wakati serikali ikilenga kuongeza mawasiliano ya intaneti nchini kwa kilomita zingine 100,000 za nyaya za faiba kupitia kwa njia ya dijitali.
Data za hivi karibuni zilizotolewa na CA zinaonyesha kwamba kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu, jumla ya mawimbi ya kimataifa ya intaneti yaliyopatikana nchini yaliongezeka kutoka 11,970.53Gbps hadi 14,413.053Gbps.
“Kumekuwa na uhamiaji mkubwa kutoka kwa sauti hadi data, miradi mipya imeasisiwa ikiwemo upanuzi wa minara mashhinani, 4G, 5G na uzinduzi wa miundombinu ya faiba,” ilisema CA katika ripoti yake ya robo mwaka.
Watumiaji wengi wameendelea kutumia simu za mkononi milioni 62.96 zinazopatikana nchini.