Uwanja wa Raila Odinga katika kaunti ya Homa Bay, uko tayari kuandaa sherehe za mwaka huu za Madaraka mnamo Juni Mosi.
Ujenzi wa uwanja huo umechukua muda wa miezi tano na unafanikisha ahadi ya Rais William Ruto kwa wakazi wa Homa Bay ya kuinua viwango vya uwanja huo wa mashabiki 12.
Akizungumza alipoongoza kamati ya sherehe za kitaifa katika ukaguzi wa uwanja huo, Katibu katika wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, alipongeza hatua zilizopigwa katika ukarabati huo, akisema uwanja huo utatumika kama kitovu cha kukuza talanta katika eneo hilo hata baada ya sherehe hizo.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi katibu Omollo alikuwa ameandamana na Waziri wa Michezo Salim Mvurya na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, miongoni mwa maafisa wengine wakuu wa serikali ya taifa na ile ya kauti hiyo.
Kwa upande wake Waziri Mvurya alifurahishwa na kazi iliyofanywa kwenye uwanja huo, akisema ukarabati wa uwanja wa Raila Odinga unaashiria ushirikiano mwema wa viongozi wa eneo hilo na humu nchini kwa jumla.
Uwanja wa Raila Odinga ni mojawapo wa viwanja ambavyo vimekuwa vikikarabatiwa pamoja na Kasarani, Nyayo, Bukhungu na Kirigiti miongoni mwa viwanja vingine, mbali na uwanja unaojengwa upya wa Talanta City.
 
					 
				 
			
 
                                
                              
		 
		 
		 
		