Waziri wa masuala ya kigeni nchini Uturuki Hakan Fidan amesema kwamba nchi yake imekatiza kabisa uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na Israel na imefungia kabisa ndege zake kulalamikia vita vya Gaza.
Akizungumza Ijumaa katika kikao maalum cha bunge la Uturuki, Fidan alisema Israel imekuwa ikitekeleza mauaji ya halaiki Gaza kwa muda wa miaka miwili sasa na kupuuza ubinadamu ulimwengu ukitazama.
Uturuki ilikatiza uhusiano wa biashara na Israel mwezi Mei mwaka jana, ikitaka kusitishwa kwa mapigano kabisa na kuingia kwa msaada wa kibinadamu mara moja Gaza. Mwaka 2023, nchi hizo mbili zilifanya biashara ya dola bilioni 7.
Ankara imekuwa ikielezea wazi wazi msimamo wake kuhusu vita vya Israel dhidi ya Gaza, huku Rais Recep Tayyip Erdogan akivitaja kuwa ni mauaji ya kimbari.
Maoni yake yanawiana na ya viongozi wengine wengi duniani na mashirika makubwa ya haki za binadamu yanayomfananisha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na kiongozi wa Ujerumani wa Kizazi cha Nazi, Adolf Hitler.
Kuhusu Syria, Ankara imeishtumu Israel kwa kuhujumu makusudi juhudi za taifa hilo kujijenga upya baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 14 na kuondolewa kwa kiongozi wa muda mrefu Bashar al-Assad kufuatia mashambulizi ya ghafla ya waasi.
Vyombo vya habari vya Uturuki viliripoti wiki iliyopita kwamba marufuku ya usafiri wa baharini unaohusiana na Israel ilikuwa imewekwa, ingawa hakukuwa na taarifa rasmi.
Kwa mujibu wa ripoti, meli za Israel zilipigwa marufuku kutia nanga Uturuki na meli zinazopeperusha bendera ya Uturuki hazikuruhusiwa kuingia katika bandari za Israel.