Mfumo wa upatanishi wa kesi nje ya mahakama, umesaidia uchumi wa taifa hili kupata takriban shilingi bilioni 52.1, kulingana na takwimu zilizotolewa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Katika taarifa ilisomwa kwa niaba yake na naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu wakati wa mkutano wa pili kuhusu upatanishi, Jaji Mkuu Martha Koome alisema kesi 16,770 kati ya kesi 18,162 ambazo ziliorodheshwa kushughulikiwa nje ya mahakama, tayari zimekamilika, hii ikiwa ni sawa na asilimia 92.3.
“Utatuaji wa kesi nje ya mahakama unaimarika zaidi kila mwaka. Katika mwaka wa kifedha wa serikali uliopita wa 2022/23, asilimia 51.2 ya kesi hizo zilishughulikiwa, huku katika mwaka huu wa kifedha wa 2023/24, asilimia 54.98 ya kesi hizo zimetatuliwa. Katika mwaka huu, huchukua siku 73 kukamilisha upatanishi wa kesi moja,” alisema Jaji Mkuu Martha Koome.
Tangu kufanyika kwa mkutano wa mwaka jana ulioangazia upatanishi katika sekta ya benki, zaidi ya kesi 400 katika sekta ya benki zimehamishwa kushughulikiwa nje ya mahakama.
Mfumo wa upatanishi wa kesi nje ya mahakama, umeanzishwa katika kaunti 40, huku juhudi zikitekelezwa kuhakikisha mfumo huo unaanzishwa katika kaunti saba zilizosalia.
Kulingana na Jaji huyo Mkuu, idadi ya wapatanishi wa kesi nje ya mahakama inaendelea kuongezeka na sasa kuna wapatanishi 1,515.