Utata waghubika kifo cha Mohbad

Marion Bosire
2 Min Read
Marehemu Mohbad, mwanamuziki wa Nigeria

Mwanamuziki wa Nigeria Mohbad aliaga dunia Septemba 12, 2023 na wengi nchini humo wametilia shaka kifo chake wakiamini kwamba aliuawa.

Video zimesambazwa mitandaoni zikionyesha mwanamzuki huyo dakika za mwisho mwisho akilia na kutaja mtu ambaye anaamini alipanga na kutekeleza njama ya kumuua.

Inasemekana kwamba Mohbad ambaye jina lake halisi ni Ilerioluwa Oladimeji Aloba alikuwa akiishi kwa hofu kubwa. Kwenye video hiyo anasikika akizungumza lugha yake ya kiasili huku akimtaja mwanamuziki mwenza Zinoleesky.

Anasema Zino ndiye alimsema na kwamba alipatiwa maji akanywa ndipo akaanza kuhisi vibaya.

Mazishi yake pia yaliharakishwa sana ilhali yeye sio wa dini ya kiisilamu ambapo mtu huzikwa siku ya kifo chake.

Jeneza lake pia lilikuwa dogo kuliko mwili wake hali ambayo ililazimu wapinde shingo yake ili atoshee humo.

Mwanabiashara aliyewauzia jeneza hilo alijotokeza mitandaoni akajiondolea lawama akisema aliharakishwa sana na waandalizi wa mazishi ya Mohbad mpaka akasahau kuitisha vipimo na akatumia vipimo vya kawaida.

Haijulikani ni nini mwanamuziki huyo alifanya ambacho anaamini mwenzake Zino alimsema na kusababisha adhuriwe.

Mwigizaji wa filamu za Nollywood Dike Osinachi – Egbeigwe Apama kwenye video alisema kwamba yeye angekuwa msimamizi wa idara ya polisi nchini humo, kuna watu angekuwa amewatia mbaroni ili kufahamu ukweli kuhusu kifo cha Mohbad.

Februari mwaka jana, Mohbad, Zinoleesky na wengine wanne walikamatwa na maafisa wa kitengo cha kupambana na mihadarati nchini Nigeria kutoka kwa makazi yao katika mtaa wa kifahari wa Lekki, jijini Lagos.

Inadaiwa kwamba walipatikana na aina mbali mbali za dawa za kulevya lakini baadaye waliachiliwa huru.

Share This Article