China inatafuta ushirikiano na sekta ya utalii ya Kenya katika nyanja za utalii endelevu huku Kenya ikitajwa kuwa mwasisi wa utalii wa vivutio vya asili barani Afrika.
Hii ni kwa mujibu wa Makamu Waziri wa Wizara ya Utamaduni na Utalii ya China, Lu Yingchuan.
Akizungumza wakati wa Mazungumzo ya Utalii kati ya Kenya na China na Kampeni ya Kukuza Utalii ya “Hello China” katika Hifadhi ya Maasai Mara, Lu alipongeza juhudi za Kenya zinazolenga kuhakikisha inasalia kivutio nambari moja cha watalii barani Afrika.
“Kenya, kama moja ya waasisi wa utalii wa vivutio asili barani Afrika, imepata tajriba kubwa katika kuunganisha utunzaji wa ikolojia na uendelezaji wa utalii,” alisema Lu.
“Mabadilishano na ushirikiano wa utalii kati ya nchi zetu mbii unajivunia uwezo mkubwa na mpana, kwani nchi zote mbili zina rasilimali nyingi za utalii na vivutio vya kipekee vya kitalii.”
Kenya imeboresha nafasi yake kama kinara wa utalii wa vivutio asili kutokana na shughuli mbalimbali inazofanya, wanyama pori na juhudi za uhifadhi.
Nchi hiyo ina mbuga za kitaifa za wanyama pori 23, hifadhi za kitaifa 28 na hifadhi 6 za majini na kuifanya kuwa nyumbani kwa wanyama mbalimbali wa porini kama vile simba, tembo, punda milia na spishi za ndege zaidi ya 1,070.
Makamu Waziri huyo amesisitiza utayari wa China kuimarisha mabadilishano na ushirikiano kati ya China na Kenya, kukuza na kuendeleza sekta za kitalii za nchi zote mbili na kuongeza hadi kiwango kipya Ushirikiano Mpana wa Kimkakati kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Katibu wa Utalii John Ololtuaa ailisisitiza kujitolea kwa serikali ya Kenya kuimarisha ushirikiano na China, kushirikishana urithi, ushirikiano unaoweza ukakuzwa na fursa ndani ya sekta za kitalii na kitamaduni.
Aliyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na kaimu Katibu wa Utalii Benard Kahuthia.