Hali ya usalama imeimarishwa kote nchini kabla ya maandamano yaliyopangwa na muungano wa upinzani, Azimio kufanyika.
Hali ya utulivu pia imeshuhudiwa katika sehemu mbalimbali za nchi huku maafisa wa usalama wakishika doria.
Huku Azimio ikisisitiza kuwa itaendelea mbele na maandamano, Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome ameyataja kuwa kinyume cha sheria na kuonya kuwa yeyote atakayepatikana akihusika katika visa vya utovu wa usalama ataadhibiwa vikali.
“Kwa mujibu wa mamlaka ya Huduma ya Taifa ya Polisi ya kudumisha sheria na mpangilio, kulinda maisha na mali na kudumisha amani, tungependa kuutarifu umma kuwa maandamano yoyote yatakayofanywa katika sehemu yoyote ya Kenya Jumatano, Julai 19 yatakabiliwa mara moja kwa mujibu wa sheria.”
Muungano wa Azimio umeitisha maandamano kulalamikia gharama ya juu ya maisha na kushinikiza kubatilishwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023.
Hata hivyo, serikali imeonya kuwa haitaruhusu kufanyika kwa maandamano yoyote nchini.
Hii ni kutokana na uharibifu wa mali na vifo vilivyotokana na maandamano yaliyoandaliwa na muungano wa Azimio wiki iliyopita.
Tume ya Utawala wa Sheria katika taarifa imeonya dhidi ya vurugu na uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya Azimio na kuwataka maafisa wa usalama kuhakikisha usalama unadumishwa.