Kamishna wa kaunti ya Baringo Stephen Kutwa, amesema maafisa 2,000 wa usalama, wamepelekwa katika maeneo tofauti ya kaunti hiyo, kuhakikisha mtihani wa KCSE unafanywa katika mazingira salama.
Akizungumza na wanahabari katika afisi yake siku ya Jumatano, Kutwa alidokeza kuwa maafisa wa asasi mbali mbali za usalama na wale wa elimu, wamepewa maagizo kuhakikisha miongozo yote ya baraza la mitihani hapa nchini(KNEC), inafuatwa kikamilifu.
Kulingana na kamishna huyo, watahiniwa 15,502 wanafanya mtihani wa KCSE katika vituo 98 vya mitihani katika kaunti ndogo saba za eneo hilo, huku watahiniwa 17,905 wanatarajiwa kufanya mtihani wa KPSEA katika vituo 758 vya mitihani.
Hata hivyo aliongeza kuwa wanafunzi watatu watafanyia mitihani yao wakiwa gerezani.
Aidha alidokeza kuwa maafisa zaidi wa usalama wamepelekwa katika vituo vya mitihani vilivyoko katika maeneo yanayokabiliwa na hatari ya usalama.
Aliongeza kuwa hakuna mwanafunzi ataruhusiwa kufanyia mtihani nje ya kituo chake kama ilivyoshuhudiwa hapo awali, kutokana na changamoto kama vile mafuriko au utovu wa usalama.