Ndege kubwa ya Urusi ya kurusha mabomu ya masafa marefu imeharibiwa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine, kulingana na ripoti.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha ndege ya Tupolev Tu-22 ikiwaka moto kwenye uwanja wa ndege wa Soltsy-2, kusini mwa St Petersburg.
Moscow ilisema kuwa droni isiyokuwa na rubani ilipigwa na moto wa silaha ndogo lakini iliweza “kuharibu” ndege hiyo. Ukraine haijatoa maoni.
Baadaye, walinzi wa anga wa Urusi walidungua ndege mbili zisizo na rubani katika mkoa wa Moscow, Meya Sergei Sobyanin alisema.
Maafisa wa ulinzi walisema ndege nyingine mbili zisizo na rubani zilinaswa kwenye eneo la Bryansk, kaskazini-mashariki mwa mpaka wa Ukraine.
Safari za ndege zilisitishwa katika viwanja vya ndege vitatu vikubwa zaidi vya Moscow, kulingana na vyombo vya habari vya serikali – lakini viwanja vya ndege viwili vikuu vya kimataifa huko Sheremetyevo na Domodedovo vilifunguliwa tena.
Ndege ya kivita ya Urusi ya Tu-22 iliyoharibiwa inaweza kusafiri kwa kasi mara mbili ya sauti na imekuwa ikitumiwa sana na Urusi kushambulia miji ya Ukraine.
Shambulio hilo sasa linatoa taswira mpya ya uwezo wa Ukraine kushamulia malengo ndani kabisa ya Urusi.
Kyiv katika miezi ya hivi karibuni imezindua makumi ya ndege zisizo na rubani kushambulia Moscow, safari ya maili mia kadhaa. Soltsy-2 iko karibu maili 400 (650km) kutoka mpaka wa Ukraine.