Mabadilishano makubwa ya wafungwa kati ya Urusi na nchi za Magharibi tangu enzi ya Vita Baridi yalifanyika mapema Alhamisi, huku jumla ya takriban watu 24 waliachiliwa, Marekani imethibitisha.
Ikulu ya Marekani ilisema wafungwa 16 walikuwa wameachiliwa na walikuwa wakirejea Ulaya na Marekani. Miongoni mwao ni mwandishi wa Wall Street Journal Evan Gershkovich.
Kwa upande wake, wafungwa wanane wa Urusi wameachiliwa huru kutoka magereza nchini Marekani, Norway, Ujerumani, Poland na Slovenia, wakiwemo watu wanaotuhumiwa kwa shughuli za kijasusi.
Watoto wa wafungwa wawili pia walirudi Urusi.
Mabadilishano hayo yalifanyika kwenye barabara ya ndege katika uwanja wa ndege wa Ankara mapema Alhamisi.
Rais Joe Biden amethibitisha kuwa mwanajeshi mkongwe wa Wanamaji wa Marekani Paul Whelan, mwandishi wa habari mwenye asili ya Urusi na Marekani Alsu Kurmasheva na mwanaharakati wa Urusi mwenye asili ya Uingereza Vladimir Kara-Murza – ambaye ana ‘Green Card’ – pia wako njiani kurejea Marekani.
Makubaliano hayo yalifanyika kwa zaidi ya miezi 18 na yanaonekana kujumuisha matakwa ya Moscow ya kutaka Vadim Krasikov arejeshwe.
Alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela nchini Ujerumani kwa kutekeleza mauaji katika bustani ya Berlin, na sasa amerejea nchini Urusi.
Maafisa wakuu wa utawala wa Marekani walimtaja kama “mtu mbaya” na kusema “hakika alikuwa muhimu zaidi ambaye Warusi walitaka arejeshwe”.