Viongozi wa upinzani humu nchini wametoa makataa ya siku saba kwa Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja na Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen kuhakikisha vijana waliotekwa nyara wameachiliwa huru.
Viongozi hao wameonya kuwa iwapo agizo hilo halitatekelezwa, wataandaa maandamano makubwa ambayo yatatatiza shughuli za kawaida nchini.
Wakiongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, na mwenzake wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa, viongozi hao wameendelea kuishutumu serikali kwa madai ya kuwanyanyasa na kuwadhulumu Wakenya wanaothubutu kukosoa uongozi mbaya.
Wakizungumza walipohudhuria fainali za mashindano ya kandanda yaliyoandaliwa na Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, katika uwanja wa Chuo cha Mafunzo ya Matibabu cha KMTC Shianda, kaunti ya Kakamega, viongozi hao walisisitiza kuwa serikali ina jukumu la kuhakikisha haki na usalama wa raia wake.
Katika hotuba yake, Kalonzo alilitaka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) kuzingatia kuiondoa Kenya kama mwanachama kutokana na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea kushuhudiwa nchini.
Viongozi hao wamesema hawatakubali kuongozwa na utawala wa kiimla na wameapa kusimama kidete kulinda haki za wananchi wote bila uwoga wala upendeleo.
Taarifa ya Carolyn Necheza