Viongozi wa upinzani leo Jumatatu wanaelekea katika kaunti ya Makueni kujinadi kwa wakazi wa eneo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Upinzani unazindua ziara ya siku tano inayojulikana kama “Komboa Kenya” katika eneo la Lower Eastern.
Wakati wa ziara hiyo, utatembelea maeneo ya Tawa, Mbumbuni, Kikima, Mukuyuni, Kilala na kisha Wote Mjini.
Kinara wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa na mwenzake wa DP Justin Muturi ni miongoni mwa wanaotarajiwa kushiriki ziara hiyo.
Wengine ni Seneta mteule wa zamani Gloria Orwoba.
Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ametaja ziara hiyo kuwa mwanzo wa kampeni kali itakayoendeshwa na upinzani unaotafuta kufanya kila uwezalo kuingia madarakani katika uchaguzi ujao.
Rais William Ruto ameupuuzilia mbali upande huo akiutaja kama usiokuwa na ajenda yoyote kwa manufaa ya taifa kando na kaulimbiu zao.
Ruto anasema ataushinda upinzani debeni asubuhi na mapema kwa sababu ya kukosa mshindani wa kupigiwa mfano.