Upasuaji wa maiti ya Gatwiri wathibitisha kilichosababisha kifo chake

Marion Bosire
1 Min Read

Familia ya marehemu mwigizaji na muunda maudhui mitandoni Tabitha Gatwiri imetoa taarifa kuhusu kilichosababisha kifo chake.

Upasuaji ulifanywa katika makafani ya hospitali ya chuo kikuu cha Kenyatta na katika taarifa hiyo familia ilielezea kwamba kifo chake huenda kilisababishwa na kukosa hewa.

Huenda mwendazake alikosa hewa kutokana na jinsi alikuwa amelala na anaripotiwa pia kuwa na uvimbe kwenye obongo wake.

Hali hiyo ambayo kwa kimombo inaitwa “positional asphyxia” hutokea wakati pua na mdomo haviwezi kupitisha hewa ipasavyo au mapafu kukosa kufunguka ipasavyo na hatimaye inasababisha uvimbe huo wa ubongo.

Familia ya Gatwiri aliyeripotiwa kufariki Oktoba 31, 2024 inaendeleza mipango ya mazishi na imeahidi kutoa taarifa juu ya mipango hiyo.

Kifo cha Gatwiri kilishangaza wengi hasa waigizaji na waunda maudhui wenzake kwani alikuwa amechapisha video kwenye TikTok saa chache kabla ya kifo chake kuripotiwa.

Kakake ndiye alipata mwili wake kwenye nyumba ya kupangisha aliyokuwa akiishi na anasema kwamba alianza kupata wasiwasi wakati dadake alikosa kujibu simu zake pamoja na jumbe.

Wakati aliamua kumzuru alikutana na mwili wake.

Share This Article