Umoja wa Mataifa, UN leo Jumanne umesema una mashaka kutokana na kampeni za uchaguzi wa urais nchini Tunisia ambazo “zimekumbwa” na ukandamizaji wa upinzani.
Miaka mitatu baada kuingia madarakani, Kais Saied alichaguliwa tena kuwa Rais wa Tunisia kwa asilimia 90.69 ya kura zilizopigwa, ilitangaza ISIE, mamlaka ya uchaguzi ya nchi hiyo jana Jumatatu.
Idadi ndogo ya wapiga kura iliashiria hali kubwa ya kutoridhika katika taifa hilo la Kiarabu ambalo ni chimbuko la maasi ya kupigania demokrasia.
Saied alitarajiwa mno kuibuka mshindi wa uchaguzi huo baada ya ISIE kuzuia wagombea 14 kuwania wadhifa huo huku viongozi wengine wa kisiasa wakifungwa jela.
“Visa hivyo vinatia hofu. Kushtakiwa kwao kunaashiria ukosefu wa heshima kwa mchakato wa kisheria na hakikisho la kupata haki,” amesema Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN Volker Turk.
Taarifa yake imeelezea kuwa kati ya wagombea 17 ambao wangewania urais, ni watatu tu waliokubaliwa huku idadi kadhaa ya wagombea wa urais wakikamatwa na kuhukumiwa vifungu virefu jela kutokana na mashtaka mbalimbali.
Turk alitoa wito kwa mamlaka za Tunisia kulinda michakato ya demokrasia ya nchi hiyo na kudumisha uhuru wa kimsingi.