Wadau muhimu ambao pia ni washirika wa mpango wa Mama Taifa wa mashamba madogo ya vyakula vya kutumia nyumbani almaarufu “Mama’s Kitchen Garden Initiative,” leo Alhamisi waliandaa mkutano wa kiamsha kinywa jijini Nairobi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wakuu serikalini na wale wa sekta ya kibinafsi ili kujadili mustakabali wa mpango huo uliopatiwa jina la “Mama Kitchen Garden Initiative”.
Mpango huo unalenga kukabiliana na ukosefu wa chakula na utapiamlo.
Katika hotuba yake, Katibu wa Idara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh aliangazia umuhimu wa suluhisho za mashinani katika kushughulikia changamoto zinazozidi kuongezeka za lishe humu nchini.
Ronoh alisisitiza kwamba viwango vya ukosefu wa usalama wa chakula hasa katika maeneo ya mashinani vinazidi kuwa vibaya, hasa katika maeneo hayo ambayo vyakula vya lishe bora ni vichache.
Katibu huyo alisema kwamba mpango wa Mama Taifa wa mashamba madogo kwa ajili ya chakula cha kutumia nyumbani ni suluhisho endelevu, kwa kuwezesha hasa kina mama kukuza vyakula vilivyo na lishe bora nyumbani.
Hatua hii alisema inawiana na mpango mpana wa usalama wa chakula na sera za kilimo nchini Kenya na unasaidia katika ukuaji wa uchumi kupitia kuwezesha jamii za mashinani.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Mama Doing Good Elizabeth Koskei, naye aliangazia kiwango cha utekelezaji wa mpango huo ambao unalenga kufikia familia milioni moja.
Alielezea pia kwamba wanalenga kutoa mafunzo kwa kina mama na vijana wapatao milioni mbili kuhusu mbinu za kilimo ambazo zinasaidia kutunza mazingira na kutoathiri tabianchi.
“Mpango wa Mama’s Kitchen Garden sio tu wa kukuza chakula, unalenga pia kukuza ustahimilivu wa kiuchumi, kuimarisha lishe bora na kuwapa uwezo kina mama na vijana.” alisema Koskei katika hotuba yake.
Kilimo hicho cha mashamba madogo ya nyumbani kinalenga pia kuimarisha upatikanaji wa chakula chenye afya, kupunguza utegemezi wa chakula ghali kisicho na lishe bora na kukuza hulka ya kujitegemea katika jamii.
Mkutano wa leo wa kiamshakinywa ulikuwa jukwaa muhimu la kuhimiza hatua za ushirikiano kati ya serikali, sekta ya kibinafsi na mashirika ya kijamii ili kuimarisha mpango huo.
Kenya inapokabiliana na changamoto za ukosefu wa chakula bora cha kutosha na utapiamlo, mpango wa Mama’s Kitchen Garden unaonekana kuwa njia ya matumaini katika kuafikia mustakabali wenye usalama wa chakula kwa Wakenya wote.