Ujenzi wa ‘flyover’ kwenye barabara ya Ngong waanza

Martin Mwanje
1 Min Read

Ujenzi wa barabara ya juu (flyover) kwenye barabara ya Ngong na Naivasha kwenye makutano ya Junction Mall katika kaunti ya Nairobi umeanza. 

Mamlaka ya Ustawishaji wa Barabara za Miji (KURA) imeelezea imani kwamba ujenzi huo utasaidia mno kupunguza msongamano wa mara kwa mara wa magari kwenye barabara ya Ngong.

Ujenzi huo unaofadhiliwa kupitia mkopo wa shilingi bilioni 3.58 uliotolewa na serikali ya Uhispania unatarajiwa kukamilika mwaka 2027.

“Mradi huu unaingiliana vema na mkakati mpana wa serikali ya Kenya Kwanza wa kuboresha miundombinu, kwa lengo la kuimarisha ukuaji uchumi wa muda mrefu na kuboresha mifumo ya uchukuzi katika maeneo ya miji,” amesema John Cheboi, Mkurugenzi Mkuu wa KURA.

KURA imeongeza jitihada za kupunguza msongamano wa magari jijini Nairobi kwa kuchukua hatua kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na upanuzi wa barabara zilizopo, uzinduzi wa Mfumo Maizi wa Uchukuzi (ITS) katika sehemu kuu za makutano na uwekaji wa miundombinu ya uchukuzi wa kasi wa mabasi (BRI).

Kufuatia kuanza kwa ujenzi wa barabara ya juu kwenye barabara ya Ngong, KURA inatoa wito kwa waendeshaji magari kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya waongozaji magari wakati wakikaribia eneo la ujenzi.

 

Share This Article