Ujenzi wa barabara kote nchini umekwama, asema Waziri Mbadi

Martin Mwanje
1 Min Read

Wakenya huenda wakaendelea kustahimili matatizo wanayokumbana nayo wakati wakisafiri au kusafirisha bidhaa zao kutokana na kuharibika kwa barabara nyingi nchini.

Hii ni baada ya Waziri wa Fedha John Mbadi kukiri kuwa ujenzi wa barabara kote nchini umekwama kutokana na ukosefu wa fedha.

Mbadi amesema ujenzi wa barabara hizo umetokana na hatua ya wanakandarasi kusitisha shughuli zao ili kuishinikiza serikali kuwalipa fedha zao.

“Tuko kwenye mpango na mkakati wa kuhakikisha kwamba, hasa katika sekta ya barabara, wanakandarasi wanarejea na kuendelea na ujenzi wa barabara,” amesema Waziri Mbadi alipofika mbele ya bunge la Seneti leo Jumatano kujibu maswali mbalimbali ya Maseneta.

“Tumefanikiwa kuomba mkopo kutoka kwa serikali ya China, kupitia Benki ya Maendeleo ya China, wa shilingi bilioni 36 kuendelea na ujenzi wa takriban barabara 15 ambazo zilikuwa zinajengwa kupitia fedha za serikali lakini zikakabidhiwa wanakandarasi wa China.”

Wakenya wamekuwa wakilalamikia kuharibika kwa barabara nyingi nchini, hali ambayo imesababisha matatizo ya usafiri.

Na huku serikali ikikiri kuwa ujenzi wa barabara hizo umekwama kutokana na ukosefu wa fedha, haijulikani ni lini hasa masaibu yao yatafikia kikomo.

Share This Article