Timu za Uingereza na Ufaransa zimefuzu kwa raundi ya 16 ya kombe la bara Ulaya baada ya kutoka sare kwenye mechi za mwisho za makundi.
Katika sare ya bao moja kwa moja baina ya Ufaransa na Poland ugani Signal Iduna Park, Kylian Mbappé na Robert Lewandoski walifunga kupitia mikwaju ya adhabu mnamo dakika ya 56 na 79 mtawalia.
Nayo Uingereza licha ya kuwa na wachezaji nyota k.v. Harry Kane wa klabu Beyern Munich, iliambulia yai kwa yai na Slovenia.
Mataifa mengine yaliyofuzu moja kwa moja ni Denmark na Austria. Denmark waliishia sufuri kwa sufuri na Serbia huku Austria wakiwaadhibu Uholanzi kwa magoli matatu kwa mawili. Matatu hayo yalitingwa na Donyell Malen (aliyejifunga), Romano Schmid na Marcel Sabitzer dakika ya 6, 59 na 80 mtawalia. Magoli ya Uholanzi yalipachikwa wavuni kupitia Cody Gakpo na Memphis Depay dakika ya 47 na 75.
Awamu hii ya makundi itakamilika leo Jumatano wakati ngarambe nne za kundi E na F zitakaposakatwa. Saa moja usiku, Slovakia itakabana na Romania huku Ukraine ikimenyana na Ubelgiji. Saa nne usiku, Georgia itakabiliana na Ureno wakati Uturuki ikipambana na Jamhuri ya Czech.