Ugonjwa wa kipindupindu wazuka katika baadhi ya maeneo nchini

Kaunti ambazo zimeathirika ni Migori, Kisumu na Nairobi.

Marion Bosire
2 Min Read
Aden Duale, Waziri wa Afya

Wizara ya Afya imethibitisha kuzuka kwa maradhi ya kipindipindu katika baadhi ya maeneo ya nchi hii.

Maeneo yaliyoathirika ni ya kaunti za Migori, Kisumu na Nairobi ambapo jumla ya visa 97 vimeripotiwa nikiwemo vifo vya watu sita.

Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaoambukiwa kupitia maji machafu au chakula kichafu na unaweza kusababisha vifo iwapo hautatibiwa haraka.

Dalili zake ni pamoja na kuhara, kutapika, maumivu ya viungo na ukosefu wa maji mwilini.

Katika taarifa waziri wa Afya Aden Duale alitoa takwimu la mlipuko huo wa hivi punde zaidi wa kipindupindu ambapo alisema hali ilikuwa tete kufikia Aprili 6, 2025.

Katika kaunti ya Migori visa 53 vya ugonjwa huo vimeripotiwa pamoja na kifo cha mtu mmoja, huku maeneo yaliyoathirika zaidi yakiwa Suna Mashariki, Suna Magharibi, Kuria Mashariki na Kuria Magharibi.

Kisumu visa vilivyogunduliwa humo ni 32, vifo vinne huku kaunti ndogo za Nyando na Muhoroni zikiripotiwa kuathirika zaidi.

Visa 12 na kifo kimoja vimeripotiwa Nairobi na maeneo ambayo yametajwa kama yaliyoathirika ni Kasarani, Kibra na Dagoretti Kusini.

Wizara ya afya inashirikiana na serikali za kaunti katika kushughulikia chamko hili la kipindupindu kwa lengo la kukomesha msambao.

Mikakati inayotumiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa kiwango cha juu, usimamizi faafu wa wagonjwa, kuhusisha jamii na kuhimiza usafi wa hali ya juu hasa wa maji ya kutumia nyumbani.

Wahudumu wa Afya wanapokea mafunzo kuhusu jinsi ya kushughulikia walioambukizwa kipindipindu kwa njia mwafaka huku vifaa hitajika vikisambazwa ili kutoa uhamasisho katika jamii zilizoathirika.

Wakenya wamehimizwa wazingatie Afya ya kibinafsi, wanywe maji safi na salama pekee, watunze chakula vyema na kutafuta huduma za matibabu iwapo watahisi dalili za ugonjwa huo.

Waziri Aden Duale, hata hivyo amehakikishia wakenya kwamba serikali imejiandaa vilivyo kushughulikia mlipuko huu wa kipindupindu huku akiwataka wawe macho.

Website |  + posts
Share This Article