Uganda yatuma wanajeshi zaidi Sudan Kusini

Uganda imeongeza wanajeshi zaidi baada ya wengine kupelekwa huko mwaka 2013.

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali ya Uganda imetuma wanajeshi zaidi nchini Sudan Kusini ikiwa nyongeza kwa wale ambao awali walitumwa kulinda usalama jijini Juba.

Oparesheni hiyo iliyopatiwa jina la “Mlinzi wa Kimya” inalenga kusaidia serikali ya Sudan Kusini kufuatia mvutano unaoshuhudiwa kati ya Rais Salva Kiir na maafisa wakuu serikalini waaminifu kwa Riek Machar.

Mvutano umekuwa uliongezeka nchini Sudan Kusini kufuatia hatua ya serikali ya kukamata mawaziri wawili na wakuu kadhaa wa jeshi ambao ni waaminifu kwa Riek Machar.

Kukamatwa kwa viongozi hao kulisababisha vurugu katika mji wa kaskazini wa Nasir, na kutishia kurejesha tena vita kama ilivyoshuhudiwa nchini humo mwaka 2013 hadi 2018.

Hali ya sasa inatishia kusambaratisha mapatano kati ya Kiir na Machar ambayo yalikomesha vita ambavyo vilisababisha mauaji ya watu zaidi ya laki nne.

Mkuu wa jeshi la Uganda Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais kuhusu oparesheni spesheli alisema kwamba jaribio lolote dhidi ya Rais Salva Kiir ni sawa na kutangaza vita dhidi ya Uganda.

Wanajeshi wa Uganda walipelekwa nchini Sudan Kusini kwa mara ya kwanza mwaka 2013 punde baada ya vita kuzuka nchini humo kutokana na hatua ya Kiir na Machar kung’ang’ania madaraka.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *