Kenya na Uganda zimetia saini mkataba wa pande tatu ili kuwezesha uagizaji wa bidhaa za petroli nchini Uganda kupitia bandari ya Mombasa.
Nchi hizo mbili pia zilikubaliana kujengwa kwa pamoja bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Kampala.
Rais William Ruto alisema upanuzi wa bomba hilo utarahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili na vile vile kuimarisha zaidi uhusiano uliopo kati yao.
Alikariri kwamba mkataba huo utaiwezesha kampuni ya mafuta ya Uganda National Oil kuagiza mafuta yaliyosafishwa moja kwa moja kutoka kwa watoaji mafuta katika maeneo mbali mbali,na hivyo basi kumaliza changamoto zinazoikumba sekta ya mafuta ya Uganda.
Akiongea wakati wa mkutano wa pamoja na wanahabari katika ikulu ya Nairobi,Rais Ruto pia alimpongeza Rais mwenzake wa Uganda kwa juhudi zake za kujenga jumuia ya Afrika mashariki iliyo thabiti.
Alimshukuru Rais Museveni kwa hatua ya Uganda kumuunga mkono mwaniaji wa wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika Kutoka Kenya.
Rais Museveni alitoa wito wa kuunganishwa kwa mataifa ya Afrika Mashariki kuwa shirikisho moja akisisitiza kwamba hii itasaidia kuimarisha usalama katika kanda hii.