Ufaransa,Ubelgiji na Ureno zilifuzu kwa fainali za kombe za la Euro za mwaka 2024 baada ya kusajili ushindi katika mechi za Ijumaa usiku.
Ufaransa ikicheza ugenini mjini Amsterderm uwanjani Johan Cruijff iliwabwaga Uholanzi mabao 2-1 katika kundi B,Kylian Mbappe akifunga bao moja katika kila kipindi naye Quilindschy Hartman akawafungia wenyeji bao la kufutia machozi.
Le Blues wanaongoza kundi B kwa alama 18,wakifuatwa na Ugiriki kwa pointi 12, baada ya kuwashinda Ireland mabao 2 kwa nunge Ijumaa ,wakati Uholanzi ikishikilia nafasi ya tatu kwa alama 9.
Ubelgiji ikicheza ugenini mjini Vienna ,iliwashinda Austria mabao 3-2 katika kundi F na kufuzu kwa fainali za mwaka ujao kwa mara ya tatu mtawalia .
Ubelgiji maarufu kama Red Deveils walikuwa wakiongoza magoli 3 kwa bila Dodi Lukebakio akibusu nyavu mara mbili naye Romelu Lukaku akoongeza moja kunako dakika ya 58.
Hata hivyo almanusra Ubelgiji wapoteze alama tatu baada ya Konrad Laimer, kukomboa la kwanza dakika ya 72 naye Marcel Sabitzer akapachika la pili katika dakika ya 84 kupitia mkwaju wa penati.
Ubelgiji wanaongoza kundi hilo kwa alama 16 ,pointi 3 zaidi ya Austria huku Sweeden ikishikilia nafasi ya tatu kwa alama 6.
Ureno wakicheza nyumbani walikuwa na kibarua kigumu kabla ya kuwapiku Slovakia magoli 3-2 katika kundi J, Christiano Ronaldo akipiga mabao mawili naye Goncalo Ramos akaongeza moja,David Hancko na Stanislav Lobotka wakiwafungia wageni.
Ureno wanaongoza kundi J kwa pointi 21 ikifuatwa na Slovakia na Luxemborg kwa alama 13 na 11 mtawalia.
Mataifa manne yamefuzu kwa kipute hicho ni wenyeji Ujerumani,Ufaransa,Ubelgiji na Ureno.