Ufadhili wa elimu ya juu: Serikali yawaondolea wanafunzi hitaji la kitambulisho cha kitaifa

Martin Mwanje
2 Min Read

Wanafunzi wa vyuo vikuu na mafunzo ya elimu ya juu wanaotarajiwa kuanza masomo yao mwezi ujao na hawajatimiza umri wa miaka 18 hawana tena haja ya kuhofu.

Hii ni baada ya serikali kuwaondolea hitaji la kuwa na kitambulisho cha kitaifa ili kupata ufadhili kutoka kwa serikali.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayekosa ufadhili wa kujiunga na vyuo vikuu na mafunzo ya elimu ya juu kwa kunyimwa ufadhili kwa sababu ya kukosa kitambulisho cha kitaifa.

Uamuzi huo uliidhinishwa leo Jumanne wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri ulioongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu Ndogo ya Kakameg.

Uamuzi wa Baraza la Mawaziri utapokelewa vyema na wanafunzi zaidi ya 2,000 wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu na mafunzo ya elimu ya juu na ambao hawana kitambulisho cha kitaifa kwanii hawajatimiza umri wa miaka 18.

Awali, wengi walielezea mashaka baada ya wanafunzi hao kushindwa kutuma maombi ya ufadhili kutoka kwa serikali baada ya kufungiwa nje kwa sababu ya kukosa kitambulisho cha kitaifa.

Isitoshe, Baraza la Mawaziri limeielekeza Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na washikadau wengine kuharakisha mchakato wa utoaji ufadhili kwa wanafunzi wanaostahiki wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu na mafunzo ya elimu ya juu kuanzia mwezi ujao.

Na ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu ya juu kote nchini, Baraza la Mawaziri pia liliidhinisha kupandishwa kwa vyuo 13 vya kiufundi hadi hadhi ya kuwa vyuo anuwai vya kitaifa.

 

Share This Article