Uenyekiti wa AUC: Vijana wa Afrika wamuunga mkono Raila

Tom Mathinji
2 Min Read

Muungano wa mashirika ya vijana na makundi ya wadau kutoka bara Afrika, yameunga mkono uwaniaji wa Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.

Katika taarifa ya pamoja, vijana hao walimpongeza waziri huyo mkuu wa zamani wakimtaja mwenye maono na aliye na tajiriba katika utumishi wa umma barani Afrika.

Kulingana na vijana hao, tajiriba ya Raila katika wadhifa wa mwakilishi wa Muungano wa Afrika kuhusu ustawi wa miundomsingi, yanamweka katika nafasi nzuri ya kushughulikia changamoto zinazokabili bara hili, husuan ajenda ya Muungano wa Afrika ya mwaka 2063.

“Raila Odinga ana maono ya jinsi ya kulisukuma mbele gurudumu la bara Afrika. Haogopi changamoto zozote na ni mwenye matumaini,” walisema vijana hao.

Raila alipata uungwaji mkono na vijana kutoka mataifa 15 ya Afrika, yakiwemo; Sierra Leone, Kenya, Uganda, Nigeria, Cameroon, Ghana, Zambia, Tanzania, Kenya, Togo, DRC, Sudan Kusini, Msumbiji na Jamuhuri ya Afrika ya kati.

Raila anakabiliana na Mohamoud Youssouf wa Djibouti, Anil Gayan (Mauritius) na Richard Randriamandrato (Madagascar) kuwania wadhifa huo.

Wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika utakuwa wazi mwezi Februari mwaka 2025, wakati muda wa kuhudumu wa mwenyekiti wa sasa  Moussa Faki Mahamat wa Chad, utakapokamilika.

Uchaguzi wa wadhifa huo, utafanywa mwezi Februari mwakani katika mkutano wa Muungano wa Afrika.

Share This Article