Serikali kufanyia mabadiliko uendelezaji wa ujuzi, asema Dkt. Muoria

Martin Mwanje
2 Min Read
Katibu wa Idara ya mafunzo ya kiufundi Dkt. Esther Thaara Muoria

Serikali imesisitiza dhamira yake ya kufanyia mabadiliko uendelezaji wa ujuzi kama nguzo muhimu ya kuwezesha kutimizwa kwa ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi kutoka chini kwenda juu, BETA.

Katibu wa Idara ya mafunzo ya kiufundi Dkt. Esther Thaara Muoria amesema mpangokazi wa sera iliyopitiwa upya utatekeleza jukumu muhimu katika utimizaji wa ajenda hiyo.

“Mpangokazi huu utatekeleza jukumu muhimu katika kuhakikisha utekelezaji mzuri wa Kutambuliwa kwa Mafunzo ya Awali, RPL bila kuwepo kwa nafasi yoyote ya mkanganyiko. Lengo letu ni kubuni mfumo unaotilia maanani ujuzi na umaizi wa kila mtu bila kujali asili yake au alikosomea,” alisema Dkt. Muoria katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Elimu ya Kiufundi John Tuwei wakati wa warsha ya uhalalishaji ya washikadau iliyofanyika mjini Naivasha.

“Ni muhimu kukumbuka kuwa mafanikio ya RPL yanategemea siyo tu sera na miongozo bali uongezaji wa uhamasishaji na kuupigia debe kwa mapana na marefu. Tunapaswa kufanya jitihada za pamoja za kufanya uhamasishaji juu ya Kutambuliwa kwa Mafunzo ya Awali na mafao yake miongoni mwa washikadau wote wakiwemo wanafunzi, waajiri, watoaji mafunzo na umma kwa jumla. Kadiri watu wanavyofahamu thamani ya RPL, kadiri mafunzo hayo yatakavyopokelewa.”

Wizara ya Elimu kupitia kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kufuzu Nchini, KNQA pamoja na washikadau wengine wamekuwa wakishughulikia mchakato wa mapitio hayo.

Kwa mujibu wa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KNQA Dkt. Alice Kande, hatua ya kupitia upya sera hiyo ni kuifanya iwiane na ajenda ya kitaifa na dunia.

Ripoti ya jopo la Rais kuhusu Mageuzi ya Elimu Nchini (PWPER) iliyotolewa mwezi Agosti mwaka huu ilipendekeza utekelezaji wa Kutambuliwa kwa sera ya Mafunzo ya Awali nchini.

Share This Article