Urusi yakosa kufichua iwapo Putin atahudhuria mazungumzo ya amani

Msemaji wa afisi ya Rais Dmitry Peskov alisema anasubiri maagizo ya Rais Putin kabla ya kufichua orodha ya watakaokuwa kwenye ujumbe wa Urusi nchini Uturuki.

Marion Bosire
2 Min Read
Vladmir Putin, Rais wa Urusi

Afisi ya Rais wa Urusi imekosa kwa mara nyingine kudhibitisha iwapo Rais Vladimir Putin atasafiri hadi Uturuki kwa mazungumzo ya kutafuta amani kati yake na Rais wa Volodymyr Zelenskyy.

Haya yanajiri huku shinikizo za kimataifa zikizidi kuongezeka juu ya Urusi kukubali kushauriana moja kwa moja katika juhudi za kukomesha vita vya miaka mitatu nchini Ukraine.

Msemaji wa afisi ya Rais Dmitry Peskov aliambia wanahabari leo kwamba serikali itafichua walio katika ujumbe wa Urusi utakaokuwa Uturuki kwa mazungumzo hayo mara tu Putin atakaporidhia.

Hata hivyo Peskov alithibitisha kwamba ujumbe wa Urusi utakuwa ukisubiri ule wa Ukraine jijini Istanbul Mei 15.

Mazungumzo hayo huenda yakawa ya kwanza ya moja kwa moja kati ya viongozi wa Urusi na Ukraine tangu mwaka 2022, muda mfupi baada ya Urusi kuvamia jirani yake Ukraine.

Zelenskyy kwa upande mwingine alikuwa anatarajiwa kuelekea Uturuki kwa mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan leo au kesho.

Awali alitoa changamoto kwa mwenzake wa Urusi kukutana naye huko Uturuki kama ishara ya kujitolea kwake kutafuta amani ya kudumu.

Rais Zelenskyy alitoa wito pia kwa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye yuko katika ziara ya eneo la Mashariki ya Kati kufika Uturuki kushiriki mazungumzo hayo.

Mapema leo Trump alisema kwamba kuna uwezekano kwamba atafika Uturuki iwapo Putin naye atakuwepo.

Website |  + posts
Share This Article