Chama tawala cha UDA na kile cha ODM vitafanya mkutano wa pamoja wa wabunge wake wiki ijayo.
Hayo yametangazwa na Baraza la Kuu la ODM, NEC, leo Jumatano.
Kwa mujibu wa baraza hilo, mkutano huo utaandaliwa Machi 10 ili kujadili ripoti yenye hoja 10.
Vyama hivyo vitakutana wakati ambapo hali ya vuta ni kuvute imeibuka katika chama cha ODM, kiini cha tofauti hizo kikiwa ushirikiano kati ya chama cha Chungwa na UDA.
Huku mrengo wa kaimu kiongozi wa ODM Dkt. Oburu Oginga ukielezea utayari wa kushirikiana na utawala wa Rais William Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, ule unaoongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna unapinga vikali hatua hiyo.
Kiasi kwamba baadhi ya wanachama wa mrengo wa Sifuna, akiwemo mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino umetaka kuitishwa kwa mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa ODM, NDC kuamua uongozi wa halali wa chama hicho kufuatia kifo cha kinara wake Raila Odinga.
Ni mkutano ambao kiongozi wa wachache katika Bunge la Taifa Junet Mohammed anasema wako tayari kuandaa mkutano huo baadaye mwezi huu.
Kwenye mkutano huo, wajumbe wanatarajiwa kupiga kuchagua viongozi wa chama hicho huku Sifuna ambaye pia ni Seneta wa Nairobi na wandani wake wa kisiasa wakilengwa kutemwa chamani.