Serikali imepiga marufuku uchimbaji madini katika kaunti ya Siaya, kama hatua ya kuzuia maafa wakati wa msimu wa mvua za El Nino.
Kamishna wa kaunti ya Siaya Jim Njoka, asasi za usalama za kaunti na kaunti ndogo, kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa.
Akihutubia wananchi wakati wa sherehe za Mashujaa, Njoka alisema kaunti ya Siaya ni maarufu sana kwa kuporomoka kwa migodi na kusababisha maafa, shughuli ambayo haitakubalika.
Alisema hatakubali kuendelea kwa shughuli ambazo zinasababisha kupotea kwa maisha katika eneo hilo.
Na huku msimu wa mvua ukianza, Njoka aliwataka wanaoishi katika maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko mara kwa mara, kuhamia maeneo salama, akidokeza idara ya utabiri wa hali ya hewa ilitoa tahadhari mapema.
Akiguzia swala la usalama, kamishna huyo wa kaunti alisema maafisa wa usalama wametekeleza wajibu wao ipasavyo, na kamwe visa vya uhalifu havitavumiliwa. Aliwaonya raia dhidi ya kuchukua hatua mikononi mwao.
Sherehe za Mashujaa kaunti ya Siaya ziliandaliwa katika uwanja wa chuo cha mafunzo ya utabibu, KMTC.