Chama cha UDA kitaanda uchaguzi wa mashinani katika awamu nne kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.
Uchaguzi huo utafanywa kwa njia ya elektroniki katika hatua ambayo inadhamiria kuhakikisha unakuwa na uwazi wa hali ya juu na kuepusha mafarakano ambayo hukumba chaguzi kama hizo.
Katika taarifa iliyosomwa na mwenyekiti wa UDA Cecil Mbarire, imebainika kuwa Aprili 26, chama hicho kitaandaa awamu ya kwanza ya uchaguzi wa mashinani katika kaunti za Nairobi, Narok, Pokot Magharibi, Busia, Homa Bay, Isiolo na Garissa.
Katika awamu ya pili itakayoandaliwa Juni 22, uchaguzi huo utafanywa katika kaunti za Mombasa, Uasin Gishu, Nyandarua, Tharaka Nithi, Machakos, Kisii, Bungoma, Siaya, Taita Taveta, Wajir, Tana River, Kwale na Marsabit.
Awamu ya tatu ya uchaguzi huo imepangwa kuandaliwa Agosti 10 katika kaunti za Kiambu, Embu, Kericho, Meru, Migori, Kakamega, Nyamira, Kitui, Elgeyo Marakwet, Samburu, Kajiado, Mandera, Kilifi, Murang’a na kaunti ya Lamu.
Awamu ya nne na ya mwisho itaandaliwa Agosti 24 katika kaunti za Nakuru, Bomet, Nyeri, Kirinyaga, Nandi, Baringo, Turkana, Laikipia, Trans Nzoia, Kisumu, Vihiga na Makueni.
“Punde baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa mashinani katika kaunti zote, chama cha UDA kitaandaa uchaguzi wa kaunti na wa kitaifa kufikia mwezi Disemba mwaka huu,” alisema Mbarire ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kirinyaga akiwa ameandamana na viongozi kadhaa wa chama hicho.
Tangazo la kuandaliwa kwa uchaguzi huo lilitolewa leo Jumanne, siku ambayo Rais William Ruto aliongoza mkutano wa kamati ongozi ya kitaifa katika makao makuu ya chama cha UDA jijini Nairobi.