Uchaguzi mdogo: Ruto awapongeza washindi wakati UDA ikitamba

Chama cha UDA kiliibuka kidedea kwenye chaguzi ndogo zote nne zilizoandaliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC Februari 26.

Martin Mwanje
2 Min Read
Elphas Kainanga Shalakha, mshindi wa uchaguzi mdogo wadi ya West Kabras

Rais William Ruto ameonekana kufurahia mno matokeo ya uchaguzi mdogo uliofanywa katika maeneo manne jana Alhamisi. 

Ruto amewalimbikizia sifa sufufu wakazi wa eneo eneo bunge la Isiolo Kusini, na wadi za West Kabras, Muminji, na Evurore kwa kukiunga mkono kwa dhati chama cha UDA kwenye uchaguzi huo.

UDA ilishinda viti vyote kwenye uchaguzi huo.

Katika eneo bunge la Isiolo Kusini, Tubi Mohammed alimtema dada yake Bina Tubi na kuibuka mshindi baada ya kuzoa kura 7,352 ikilinganishwa na za Bina aliyepata kura 634 pekee.

Wawili hao ni wanawe mbunge wa zamani wa eneo bunge hilo Mohamed Tubi Bidu aliyefariki mwezi Novemba mwaka jana.

Katika wadi ya West Kabras, eneo bunge la Malava, Elphas Kainanga Shalakha wa UDA pia aliibuka mshindi na kufuata nyayo za David Ndakwa pia wa UDA aliyetangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo wa ubunge mwaka jana.

Ushindi wa hivi punde ukifasiriwa na wengi kuwa ishara kwamba eneo la Magharibi linageuka kuwa ngome ya UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Katika eneo bunge la Mbeere Kaskazini, Duncan Muratia Nyaga alitangazwa mwakilishi mpya wa wadi ya Evurore huku Peterson Njeru akishinda katika wadi ya Muminji.

“Pongezi kwa ushindi wenu na imani ambayo watu wako nayo kwenu,” alisema Rais Ruto katika ujumbe wake wa pongezi.

Share This Article