Uanachama wa Gabon katika AU wasitishwa

Marion Bosire
2 Min Read
Raia wa Gabon wakisherehekea mapinduzi ya serikali jijini Libreville

Umoja wa Afrika, AU umesitisha uanachama wa taifa la Gabon kufuatia hatua ya wanajeshi wa taifa hilo ya kupindua serikali ya Rais Ali Bongo.

Mapinduzi hayo ya serikali ya Gabon ndiyo ya nane katika eneo la magharibi na kati mwa Afrika na yanafikisha mwisho uongozi wa familia ya Bongo katika taifa hilo wa miaka zaidi ya 50.

Kufikia sasa, jeshi limemtangaza Jenerali Brice Oligui Nguema ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la ulinzi la Rais kuwa kiongozi wa taifa la Gabon na anapangiwa kuapishwa Jumatatu.

Baraza la amani na usalama la AU ndilo lilichukua hatua ya kwanza dhidi ya Gabon Alhamisi kwa kuizuia kushiriki mipango yake yote na kuendelea kuwa kwenye mashirika na taasisi za umoja huo.

Shirika la kisiasa la nchi za katikati mwa Afrika ambapo Gabon ni mwanachama, pia limekashifu mapinduzi nchini Gabon, likisema linapanga mkutano wa wanachama kupanga jinsi ya kujibu mapinduzi ya serikali nchini humo.

Maafisa wakuu katika jeshi walitangaza hatua ya kupindua serikali alfajiri ya Jumatano Agosti 30, 2023, saa chache baada ya tume ya uchaguzi ya Gabon kumtangaza Ali Bongo kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais ambao ulikuwa umeandaliwa Jumamosi. Bongo alikuwa anaanza kipindi chake cha tatu uongozini.

Siku hiyo hiyo mchana, video ya Bongo ambaye alikuwa akizuiliwa kwenye makazi yake rasmi akiomba usaidizi ilichipuza mitandaoni ambapo alielezea kwamba watu wa familia yake wako maeneo tofauti na hajui kinachoendelea.

Upande wa upinzani nchini Gabon ulishukuru wanajeshi kwa kukomesha uongozi wa Bongo. Mike Jocktane mwakilishi wa upinzani anataka wanajeshi hao wakamilishe shughuli ya kuhesabu kura zilizopigwa Jumamosi akiwa na uhakika kwamba mwaniaji wao Albert Ondo Ossa alishinda.

Share This Article