Tuzo za Trace kuandaliwa Zanzibar mwakani

Marion Bosire
2 Min Read

Waandalizi wa tuzo za Trace wametangaza kwamba awamu ya pili ya tuzo hizo za kila mwaka itaandaliwa katika kisiwa cha Zanzibar nchini Tanzania.

Awamu hiyo ya mwaka 2024, itaandaliwa Februari 24 hadi 26 mwaka 2025 na matukio yote yatapeperushwa moja kwa moja kwenye runinga.

“Tunakupeleka rasmi kwenye safari nyingine ya kusherehekea muziki muzuri na burudani ya bara Afrika na hasa wanaounda burudani hiyo.” waliandika kwenye video ya kutangaza tuzo hizo.

Waziri wa utalii kisiwani Zanzibar Mudrik Soraga na mwanzilishi mwenza wa tuzo za Trace Olivier Laouchez waliandaa kikao na wanahabari leo katika hoteli ya Mora kutangaza ujio wa tuzo hizo.

Awamu ya kwanza ya tuzo za Trace iliandaliwa katika ukumbi wa BK Arena jijini Kigali nchini Rwanda Oktoba 21, 2023.

Wanamuziki zaidi ya 50 kutoka sehemu mbali mbali ulimwenguni walitumbuiza kwenye hafla hiyo ya mwaka jana, wakiwemo Diamond Platnumz, Juma Jux na Zuchu wa Tanzania.

Wasanii waliowakilisha Kenya kwenye awamu ya kwanza ya tuzo za Trace ni Nadia Mukami na Khalighraph Jones walioteuliwa kuwania tuzo ya msanii bora Afrika Mashariki iliyotwaliwa na Diamond Platnuz.

Mukami alihusishwa pia kwenye kitengo cha mwanamuziki bora wa kike ambapo Viviane Chidid wa Senegal aliibuka mshindi.

Janet Otieno naye alikuwa ameteuliwa kuwania tuzo ya mwimbaji bora wa nyimbo za injili ambapo alishindwa na KS Bloom kutoka Ivory Coast.

Inasubiriwa kuona iwapo wasanii zaidi wa Kenya wataangaziwa kwenye tuzo za mwaka huu za Trace.

Share This Article