Rais William Ruto amesema serikali yake inajizatiti kuhakikisha taifa hili linawajumuisha wote na kuheshimu utofauti wa raia wake.
Akizungumza leo Ijumaa alipokuwa mwenyeji wa waumini wa dini ya Kiislamu kuadhimisha Siku Kuu ya Idd-uL-Fitr katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi wa taifa aliishukuru jamii ya Waislamu kwa kuliombea taifa hili, na jukumu muhimu wanalotekeleza kudumisha amani, umoja na kuimarisha nguvu ya kiroho kote nchini.
Rais Ruto alitoa wito kwa Wa-Kenya kudumisha maadili mema, ukarimu na uwiano, huku akielezea umuhimu wa siku hii katika kuimarisha Imani na utulivu nchini.
Kwenye hafla hiyo, Rais Ruto alisisitiza haja ya kutekeleza siasa zilizo na sera, kwa manufaa ya maendeleo na mshikamano wa taifa hili.
Sherehe za Idd-uL-Fitr hufanyika baada ya kukamilika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao hudumu kwa siku 30.