Waziri wa Ulinzi Aden Duale amewapongeza wahadhiri, wanafunzi na jamii kwa jumla kwa ujasiri wao na kwa kutokata tamaa hata baada ya kutokea kwa shambulizi baya zaidi la kigaidi lililosababisha maafa katika Chuo Kikuu cha Garissa.
Aprili 2, 2015, magaidi yaliingia katika chuo hicho cha kipekee katika eneo la Kaskazini Mashariki na kuua watu 148, wengi wao wakiwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufuzu kwa wanafunzi iliyoandaliwa katika uwanja wa chuo hicho jana Alhamisi, Duale alisema nguvu za kalamu hatimaye zimezishinda zile za silaha.
“Wanamgambo hao wakiwa na ari yao potovu walidhamiria kuhakikisha kituo hiki hakirejelei shughuli zake kamwe, lakini tunamshukuru Mwenyezi Mungu na kwa ujasiri wetu tupo hapa leo tukisherehekea kufuzu kwa wanafunzi 482 miongoni mwao wakifuzu na shahada ya uzamivu,” alisema Duale.
Waziri huyo aliongeza kuwa serikali imejitolea kuwaangamiza kabisa wanamgambo wa Al-Shabaab ambao lengo lao kuu ni kudumaza taasisi zote za kijamii.
“Nasimama hapa kama Waziri wa Ulinzi na ninataka kuwatizama wanamgambo hao ana kwa ana na kuwaambia kuwa tunawakujia. Tutatumia vikosi vyetu vya ardhini, majini, anga, na vikosi maalum kuwasaka vikali nchini Kenya na ndani ya Somalia.”
Duale alisema serikali inafanya kazi na wabia na washirika wake walio na wanajeshi nchini Somalia kwa lengo la kuliangamiza kundi hilo.
Aidha aliwataka wakazi kuungana kupigana na wanamgambo hao akisema usalama hauwezi ukaachiwa serikali pekee na kuwaonya vikali wakazi wanaoshirikiana na kundi hilo.
“Nataka kusema bayana kuwa tuna majasusi wa kutosha na tutafuatilia kila mawasiliano hasa ya wakazi wanaoshirikiana na adui yetu. Na punde ukimaliza kuwasiliana nao, tutakukamata.”
Waziri alisikitika kwamba wanamgambo hao wameazimia kutega vilipuzi barabarani wakiyalenga magari ya maafisa wa usalama na magari mengine ya umma yanayosafiria njia mbalimbali na badala yake kuwataka kukabiliana na maafisa hao moja kwa amoja.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alisema serikali itaendelea kuunga mkono masomo ya vyuo vikuu na kuitaka jamii ya eneo hilo kukilinda chuo hicho kwa hali na mali.
“Kuwa na Chuo Kikuu katika kaunti yenu ni mafanikio makubwa. Tafadhali, watu wa Garissa na Kaskazini Mashariki, kilindeni chuo hiki kwa udi na uvumba kwa sababu ikiwa kwa bahati mbaya mtakipoteza, kukipata tena haitakuwa rahisi,” alishauri Machogu.
Taarifa ya Kinyungu Kithendu