Tume ya TSC yatangaza nafasi 46,000 za ajira

Tom Mathinji
2 Min Read
Tume ya kuwaajiri walimu TSC.

Tume ya kuwaajiri walimu nchini (TSC) imetangaza nafasi 46,000 za ajira, kukabiliana na uhaba wa walimu hapa nchini. 

Kulingana na tume hiyo kupitia kwa arifa, nafasi 6,000 ni za walimu wa shule za msingi huku nafasi 39,500 zikiwaendea walimu wa shule za sekondari ya msingi.

Aidha, TSC imesema nafasi 450 zitachukuliwa na walimu wa shule za upili.

“Tume ya kuwaajiri walimu, inakaribisha maombi ya kazi kujaza nafsi 46,000 za walimu waliohitimu kwa masharti ya kudumu,” ilisema arifa hiyo ya TSC.

Ili kuhitimu kwa nafasi hizo, walimu hao wanatakiwa kuwa ni raia wa Kenya, wawe na cheti cha PI kwa wale wanaotaka kufunza shule za msingi na cheti cha diploma kwa walimu wanaotaka kufunza shule za sekondari.

Walimu wanagenzi pia wamehimizwa kutuma maombi katika kaunti, kaunti ndogo wanakotoka au katika vituo wanakofanya kazi. Tume hiyo imesema wanagenzi hao watahijatika tu kuwa na vitambulisho wakati wa mchakato wa kuwatambua.

Tume hio ilitangaza kwamba siku ya mwisho ya kutuma maombi ni Oktoba 7, 2024, wanaomezea mate nyadhifa hizo wakiagizwa kutuma maombi yao kupitia ya tovuti ya tume hiyo.

Wanaotuma maombi walihimizwa kujihadhari na matapeli wanaojisingizia kuwa maafisa wa TSC.

“Zoezi la kuwaajiri walimu halitozwi malipo yoyote. Tume hii inawaonya wanaotuma maombi dhidi ya kulaghaiwa na watu wanaojisingizia kuwa maafisa wa TSC,” ilishauri tume hiyo.

TAGGED:
Share This Article