Kenya imesisitiza kujitolea kwake katika kutekeleza malengo yaliyowekwa na kituo cha udhibiti wa magonjwa cha Africa CDC.
Aidha imekariri kujitolea kwake katika utimizaji wa maono ya pamoja katika ufanikishaji wa afya yya umma kote barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni alipokuwa akizungumza wakati wa Mkutano wa Pili unaoendelea wa Kamati ya Ushauri wa Kiufundi wa Kanda ya Afrika (ReTAC) unaoandaliwa na Africa CDC.
Muthoni alisema kuna haja kwa mataifa ya Afrika kuainisha maazimio na Utaratibu Mpya wa Afya ya Umma, unaoangazia uimarishaji wa taasisi za afya ya umma, ukuzaji wa nguvukazi yenye ujuzi wa afya ya umma, upanuaji wa utengenezaji dawa ndani ya nchi, uongezaji wa rasilimali ndani ya nchi na ukuzaji wa ushirikiano wenye vitendo.
Alitoa wito kwa mataifa ya Afrika kutoa kipau mbele kwa utengenezaji wa chanjo, uboreshhaji wa vifaa tiba na uimarishaji wa uwezo wa nguvukazi ya afya ya umma kama mikakati ya kuziba mianya iliyodhihirishwa kuwepo kutokana na janga la virusi vya korona.
Katibu huyo alisisitiza kujitolea kwa Kenya kwa mtazamo mmoja wa afya na ushirikiano na washikadau katika ngazi zote.
“Hii inaashiria kujitolea kwetu katika kuendesha upigaji hatua wenye tija na endelevu siyo tu humu nchini bali kote barani Afrika.”