Rais wa Marekani Donald Trump atalipwa dola milioni 24.5 na kampuni ya YouTube ambayo inamiliki jukwaa la mitandaoni la kuchapisha muziki na maudhui mengine.
Hii ni baada ya kiongozi huyo kuishtaki kampuni hiyo mahakamani, kutokana na hatua yake ya kumfungia akaunti yake kwenye jukwaa hilo mwaka 2021.
Wakati huo, YouTube ilihusisha uamuzi wake na ghasia zilizoshuhudiwa katika majengo ya Congress Januari 6, 2021. YouTube tayari imekubali kutoa malipo hayo.
Kampuni hiyo ya YouTube ndiyo ya mwisho kuafikia makubaliano ya kifedha na kiongozi huyo wa Marekani kati ya kampuni tatu kubwa za teknolojia ambazo alizishtaki mahakamani.
Nyingine mbili alizochukulia hatua ni Meta inayomiliki mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram, Threads, WhatsApp na Messenger pamoja na kampuni ya Twitter ambayo sasa inafahamika kama X.
Mitandao hiyo yote ilimfungia akaunti zake.
Kutoka kwa pesa atakazolipwa na Youtube, dola milioni 22 zitaelekezwa kwenye taasisi isiyo ya kiserikali ya Trust for the National Mall inayohifadhi na kuendeleza eneo la kihistoria la National Mall na kusaidia ujenzi wa White House State Ballroom huku dola milioni 2.5 zikilipwa kwa Walalamikaji wengine wakiwemo American Conservative Union.
Trump kupitia ukurasa wake wa Truth Social alijigamba kwa matokeo hayo akisema ni ushindi mkubwa unaothibitisha kuwa udhibiti wa kampuni kubwa za mawasiliano una madhara kasoro.
Kabla ya hapo Meta ilikubali kusuluhisha kesi kwa malipo ya dola milioni 25 mwezi Januari 2025 huku X ikilipa takribani dola milioni 10 mwezi Februari mwaka huu.
Majukwaa hayo ya mitandao ya kijamii yaliamua kumfungia Trump kufuatia machapisho yake kuhusu ghasia za Capitol hill ambayo yalichukuliwa kuwa hatari na ambayo yangesababisha vurugu zaidi.